WAZIRI KALEMANI AUTAKA UONGOZI WA WIZARA YA NISHATI KUFANYA KAZI KWA KASI NA UBUNIFU

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amewataka watumishi wa Wizara ya Nishati kufanya kazi kwa kasi na kwa ubunifu ili kuhakikisha sekta ya Nishati inaendelea kukua ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa maendeleo ya Viwanda na kuliletea Taifa maendeleo.

Waziri Kalemani ameyasema hayo Desemba 10, 2020 wakati akiwa kwenye kikao na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati kilichofanyika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato.

Kikao hicho cha Waziri na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati, kilichohudhuriwa na Naibu Waziri Mhe. Stephen Byabato, kimelenga kutambulisha viongozi wa Wizara hiyo na kutoa maelekezo yanayolenga kuwa na utekelezaji mzuri wa malengo yaliyowekwa katika Sekta ya Nishati.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kalemani ameiagiza Menejimenti ya Wizara hiyo kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika na wa kutosha unazalishwa nchini kutoka kwenye vyanzo vya gharama nafuu hasa maji.

Pia, ameitaka Menejimenti ya Wizara ya Nishati, kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya kusafirishia umeme kutoka kona zote nne unakamilika kwa wakati na kuwe na mtandao wa njia ya kusambazia umeme kwa kona zote nne kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi.

Vilevile, Waziri Kalemani, ameuagiza uongozi wa Wizara ya Nishati, kuhakikisha kuwa vijiji vyote 2884 ambavyo havijaunganishwa na umeme, ifikapo mwezi Desemba 2022, viwe vimeunganishwa na huduma hiyo.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, ameahidi kutoa ushirikiano mzuri na kufanya kazi kwa weledi katika kuhakikisha majukumu ya Waziri wa Nishati yanafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMSHUSHA MAMA NDOO KICHWANI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.