TAARIFA MUHIMU KUTOKA TANESCO

• INAHUSU UFAFANUZI WATAARIFA ZILIZOTOLEWA MTANDAONI KUHUSU:

– TATIZO LA KUKATIKA MARA KWA MARA UMEME MKOANI RUVUMA

Ad

– BODI YA WAKURUGENZI YA TANESCO

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kutoa ufafanuzi Juu ya taarifa iliyotolewa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO imesikitishwa na matumizi madogo ya umeme hali inayopelekea kukatika umeme Mkoani Ruvuma.

TANESCO inaufahamisha Umma kuwa mnamo tarehe 9 Machi, 2019 Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ikiwa katika ziara kukagua mradi wa Makambako-Songea, ilikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ambapo vyombo vya habari pia vilikaribishwa.

Katika kikao hicho, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, pamoja na masuala mengine muhimu yanayohusu miradi kabambe ya umeme inayotekelezwa nchini, pia walipata wasaa wa kumweleza Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa njia ya Usafirishaji umeme ya Msongo wa Kilovolti 220 Makambako – Songea ambao umemaliza kabisa matatizo ya umeme kwa Mkoa wa Ruvuma.

SABABU MBALIMBALI ZINAZOPELEKEA KUKATIKA KWA UMEME

Mosi, Umeme unaweza kukatika kutokana na hitilafu katika Mashine za kuzalisha umeme.

Pili Umeme unaweza kukatika kutokana na hitilafu kwenye njia za usafirishaji au kusambaza umeme kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kukatika kwa waya kunako sababishwa na kuangukiwa na miti au nguzo kuanguka kutokana na sababu mbalimbali.

Tatu, Umeme unaweza kukatika kutokana na kuzidiwa (overload) kwa njia za usafirishaji au usambazaji umeme.

Nne, Umeme unaweza kukatika kutokana na wateja kuwa na matumizi madogo ikilinganishwa na umeme unaofika kwenye kituo kinacho mhudumia (overvoltage).

Miundombinu yote ya TANESCO inadhibitiwa na vifaa ambavyo vimewekwa katika kiwango maalum ambacho kikizidi au kikipungua kifaa hicho hukata umeme ili kulinda kifaa hicho.

Hali halisi katika Mkoa wa Ruvuma kupitia Mradi wa Makambako Songea ni kwamba; Mradi wa ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovolti 220 Makambako – Songea umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni:-

Ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme ya msongo wa kilovolti 220 Makambako hadi Songea ambao umekamilika kwa asilimia mia moja

Ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme vya Makambako, Madaba na Songea.

Pia umekamilika kwa asilimia mia moja .

Ujenzi wa kilometa 900 za njia za usambazaji umeme katika vijiji 122 vilivyopo katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma ambao matarajio ni kuunganisha wateja wapatao 22,700 lakini hadi sasa ni wateja 7035 tu ndio waliounganishwa umeme (Sehemu hii ya mradi bado haijakamilika ).

TANESCO Inatarajia kwamba baada ya sehemu ya tatu ya mradi kukamilika na wateja kuongezeka matumizi ya umeme pia yataongezeka.

TANESCO inatoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Wadau wengine wa maendeleo kwa kuhamasisha uwekezaji wa viwanda Mkoani Ruvuma kwa kutumia nishati ya umeme.

Kwa upande wake, TANESCO inauhakikishia Uongozi na Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuwa itaendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme ili Wana Ruvuma waeendelee kupata huduma bora.

Haikuwa nia ya TANESCO wala Bodi kusababisha mkanganyiko uliojitokeza.

Uongozi unaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.

Tovuti: www.tanesco.co.tz

Twitter, www.twitter.com/tanescoyetu,

 Facebook https://www.facebook.com/tanescoyetultd/

Taarifa hii imetolewa na

OFISI YA UHUSIANO

TANESCO MAKAO MAKUU

MACHI 13, 2019

Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI KAIRUKI AWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *